in ,

CHADEMA yabadili gia angani

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na NCCR-Mageuzi vimethibitisha kuwa vitashiriki mkutano wa Kituo cha Demokrasia Tanzania baada ya hoja tano walizokuwa wakizilalamikia kuanza kufanyiwa kazi, ikiwemo kuachiwa kwa Freeman Mbowe.

Awali vyama hivyo vilisema havitoshiriki shughuli yoyote ya kisiasa ikiwemo zinazoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kwa madai ya hoja zao kutokufanyiwa kazi.

“Kwa msingi huo hatutokuwa na sababu ya kutokushiriki mkutano wa majadiliano ya amani kule Dodoma,” amesema Mkuu wa Idara ya Uenezi na Uhusiano wa Umma wa NCCR-Mageuzi, Edward Simbeye.

Hoja nyingine waliyoitaka ambayo inafanyiwa kazi ni kufanyika kwa mkutano mdogo wa wawakilishi wa vyama vya siasa kabla ya mkutano wa mwisho wa mwezi. Hilo limekubaliwa na mkutano utafanyika Machi 18, ambapo Rais Samia atakuwepo na kila chama kitatuma mwakilishi.

Mkurugenzi wa Itikadi, Uenezi na Mambo ya Nje wa CHADEMA, John Mrema amesema kutokana na kuachiwa kwa Mbowe, watashiriki mkutano huo huku wakiendelea kusisitiza utekelezaji wa hoja zao nyingine.

Amesema hoja zao nyingine ni katiba mpya, na kwamba wanatafuta njia sahihi ya kurejesha mchakato wake ili kuleta suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara.

Madai mengine ni kuruhisiwa kwa mikutano ya kisiasa ya hadhara, ili vyama viweze kujijenga zaidi.

Mkutano huo wa maridhiano ya umoja wa kitaifa utafanyika Machi 30 na 31 jijini Dodoma ukiwashirikisha pia Rais wa Tanzania, Samia Suluhu na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi.

Rwanda yatafakari kuitoza kodi Netflix

Rais Samia aagiza kuandaliwa kanuni za mikutano ya vyama vya siasa