Tanzania na Rwanda zatia saini hati ya makubaliano ya uimarishaji mpaka

0
2

Tanzania na Rwanda zimetiliana saini Hati ya Makubaliano (MoU) ya uimarishaji mpaka wa Kimataifa baina ya nchi hizo mara baada ya kukamilika kwa Kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu (JTC) kati ya Tanzania na Rwanda kilichofanyia katika mji wa Ngara mkoa wa Kagera.

Utiaji saini makubaliano hayo umefanywa kati ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Hamdouny Mansour na Abel Buhungu ambaye ni kiongozi wa ujumbe kutoka nchini Rwanda.

Akizungumza mara baada ya utiaji saini makubaliano hayo, Hamdouny Mansour, ameshukuru kwa hatua iliyofikiwa ya kutiwa saini makubaliano ya uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Rwanda na kueleza kuwa, ni matumaini yake maazimio yaliyofikiwa yatatekelezwa kama walivyokubaliana.

Naye, kiongozi wa ujumbe wa Rwanda ambaye ni Mkuu wa Ubalozi wa Rwanda nchini Sudan, Abel Buhungu ameshukuru serikali ya Tanzania kwa kuialika nchi yake kushiriki kikao cha pamoja cha uimarishaji mpaka wa kimataifa kwa nchi hizo mbili na kueleza kuwa, hana mashaka kwa kazi iliyofanyika muda si mrefu watafikia malengo yaliyokusudiwa.

Wakati wa kikao cha JTC, wajumbe walipata fursa ya kukagua mpaka wa wa kimataifa wa Tanzania na Rwanda ambapo ukaguzi ulianzia katika alama ya mpaka ya Mafiga Matatu (Kasange) mahali ambapo mto Kagera/Akagera unakutana na mto Mwidu kisha kuelekea Rusumo mahali ambapo Mto Kagera unakutana na mto Ruvuvu/Ruvubu.