Sakata la kuvuliwa uanachama wabunge 19 wa Viti Maalum wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) linaendelea kushika kasi baada ya tetesi zinazodai kuwa kuna uwezekano mkubwa wa chama hicho kupeleka majina mengine ya wabunge wa viti maalum ili kuchukua nafasi yao.
Baraza kuu la CHADEMA linakutana leo Mei 11 jijini Dar es salaam ili kujadili masuala mbalimbali yanayohusu chama hicho pamoja na uamuzi juu ya kufukuzwa kwa wabunge 19.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi tayari CHADEMA wanajiandaa kupeleka majina mengine Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo itapeleka bungeni ili kujaza nafasi zitakazoachwa wazi na wabunge hao.
Hata hivyo taarifa imeeleza kuwa majina yanayotarajia kuwarithi ni Catherine Ruge (Katibu Mkuu Bawacha), Sharifa Mohamed (Kaimu Mwenyekiti Bawacha), Suzan Kiwanga (Aliyekuwa mgombea jimbo la Mlimba, Morogoro) Grace Kiwelu, Joyce Mukya, Suzan Lyimo.
Wengine ni Devotha Minja (aliyekuwa mgombea jimbo la Morogoro Mjini) Upendo Peneza, Lucy Owenya, Rose Moshi, Rhoda Kunchela, Gimbi Masaba, Rose Mayemba, Aisha Luja, Husna Said, Nice Gisunte, Moza Ally, Dorcas Francis, Ruth Molle, Pamela Massay na Lucy Magereli.