in ,

Rais Samia kufanya ziara ya kikazi nchini Korea

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara katika Jamhuri ya Korea kuanzia Mei 30 hadi Juni 6, mwaka huu kwa mwaliko wa Rais wa Korea, Yoon Suk Yeol.

Akizungumza na waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam leo, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.) amesema katika ziara hiyo Serikali ya Tanzania na Korea Kusini zitasaini mikataba saba ya kuimarisha ushirikiano.

Amesema mkataba moja wapo unahusu msaada wa fedha kati ya Benki ya Exim ya Korea na Tanzania ambao utaiwezesha Tanzania kupata msaada na mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani Bilioni 2.5 ambao ni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka mitano ijayo yaani mwaka 2024/2028.

Pia, amesema kutakuwa na Hati ya Makubaliano kati ya Taasisi ya Utafiti wa Madini Tanzania (GST) na Taasisi ya Sayansi ya Miamba na Madini ya Korea ambayo itahusu ushirikiano katika masuala ya utafiti, uchoraji ramani na shughuli za maabara.

Aidha, amesema ziara hiyo itafuatiwa na ziara ya kikazi itakayomuwezesha kushiriki Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali Kati ya Afrika na Korea utakaofanyika Juni 3 na 4, 2024.

“Ziara hii itakuwa na sehemu kuu mbili, mosi ni ziara rasmi kati ya Tanzania na Korea, pili Rais Samia Suluhu Hassan kuhudhuria mkutano mkuu wa nchi za Afrika na Korea,” amesema Makamba.

Ameongeza kuwa, akiwa nchini humo, Rais Samia atakutana na kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais Yoon Suk Yeol yatakayofanyika tarehe 2 Juni 2024 ambapo mazungumzo hayo yatajikita kujadili namna ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Korea katika maeneo mbalimbali ikiwemo Afya, Elimu na Miundombinu.

Idadi ya wasichana wanaoambukizwa UKIMWI Zanzibar yaongezeka

Mkulima Singida aibuka na Mil. 10/- za NMB Pesa Weka na Ushinde