in ,

Balozi Togolani akanusha Tanzania kusaini mkopo Korea Kusini unaohusisha sehemu ya bahari

Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Togolani Mavura amesema Tanzania haijasaini Mkataba wowote na Jamhuri ya Korea unaohusisha Bahari ya Tanzania wala Madini katika ziara ya Rais Samia Suluhu nchini Korea.

Balozi Mavura amesema katika ziara hiyo iliyoanza Mei 31, 2024 nchini humo, Rais ameshuhudia utiwaji saini wa Mkataba mmoja pekee ambao ni mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wa dola za Kimarekani bilioni 2.5 kwa ajili ya miradi ya miundombinu.

Mbali na mkataba huo, amesema Rais Samia alishuhudia utiwaji saini wa Hati ya Maelewano (Memorandum of Understanding-MOU) mbili za Ushirikiano katika sekta za Uchumi wa Buluu na Madini ya Kimkakati.

Pia, Rais alishuhudia kusainiwa kwa Tamko la Utayari wa Kuanza Majadiliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi (Joint Statement on the launch of Negotiation on Economic Partnership Agreement-EPA).

“Tanzania na Korea wametiliana saini Mkataba mmoja; MOUs mbili, na Tamko moja,” amesema Balozi Mavura.

Aidha, ameweka wazi kuwa Tanzania haijagawa chochote kubadilishana na mkopo nafuu kutoka Korea kama ambavyo imeandikwa katika mitandao, badala yake, Tanzania inapata mkopo wa masharti nafuu kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo (EDCF) kwa mara ya tatu.

“Mara ya kwanza dola za kimarekani milioni 733 (2014-2020); mara ya pili dola bilioni 1 (2021-2025) na huu mkopo wa tatu ni dola bilioni 2.5 (2024-2028),” ameeleza huku akiongeza kuwa “Nchi 59 zilizoko barani Afrika, Asia na Ulaya zinafaidika na mkopo wa aina hii kutoka EDCF.”

Balozi Mavura amebainisha kuwa “mkopo huu wa masharti nafuu una riba ya asilimia 0.01, unalipwa kwa miaka 40, na una fungate (grace period) ya miaka 25, yaani unaanza kulipa baada ya mwaka wa 26. Hivyo si kweli kwamba mkopo huo utalipwa kwa miaka mitano.”

Mchungaji Msigwa adai Sugu hakushinda kihalali, akata rufaa

Watoto wamuua mama yao wakidai anaroga wajukuu