in ,

Padri anayedaiwa kuhusika kwenye mauaji ya mtoto albino asimamishwa kutoa huduma za kiroho

Jimbo la Katoliki la Bukoba limemsimamisha huduma za kichungaji, Padri Elipidius Rwegoshora anayedaiwa kuhusika katika mauaji ya mtoto albino, Asimwe Novart mpaka pale suala hilo litakaposhughulikiwa na vyombo vya sheria.

Taarifa hiyo imebainishwa katika gazeti la Kiongozi ambalo linatolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) ambalo limeeleza kumhoji Askofu wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Jovitus Mwijage na kueleza kuwa Padri huyo ambaye ni miongoni mwa watuhumiwa tisa wa mauaji ya mtoto albino, amesimamishwa kazi kutoa huduma za kiroho.

Akizungumza na Azam Media, Makamu Askofu, Padri Samwel Mchunguzi amelaani tukio hilo la kinyama na kueleza kwamba suala hilo liko mikononi mwa Askofu Mwijage.

“Tukio hilo kwa mtu yeyote mwenye akili timamu na aliyelelewa vizuri ni tukio ovu na hakuna mtu yeyote anayeweza kuliunga mkono [..] Kile ni kitendo cha kinyama sana na hakipaswi kufanyiwa kwa mtu yeyote yule,” ameeleza.

Mtoto Asimwe mwenye umri wa miaka miwili na nusu aliporwa mikononi mwa mama yake na watu wasiojulikana Mei 30, mwaka huu katika Kijiji cha Bulamula, Muleba mkoani Kagera, na kisha mwili wake kupatikana ukiwa umekatwakatwa na kufungwa kwenye kalavati.

Kwanini Mbappe hataruhusiwa kuvaa ‘mask’ ya bendera ya taifa kwenye mechi dhidi ya Uholanzi?

Nchi 10 za Afrika zinazoongoza kutembelewa na watalii mwaka 2024