in ,

Tanzania inaiuzia Zambia mahindi tani 650,000 kukabiliana na njaa

Tanzania inauza mahindi tani 650,000 nchini Zambia ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa kufuatia mazungumzo kati ya Rais Samia Suluhu na Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema Aprili 26 mwaka huu wakati wa ziara ya Rais Samia nchini humo pamoja na mazungumzo kati ya wizara za kisekta na balozi.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.) kupitia ukurasa wake wa X (zamani Twitter) ambapo amesisitiza kuwa Tanzania itaendelea kuwa msaada kwa washirika wake wakati wa uhitaji.Zambia imeingia makubaliano ya kununua mahindi kutoka Tanzania ili kusaidia wananchi wake zaidi ya milioni 7 wanaokabiliwa na njaa kutokana na ukame ulioikumba nchi hiyo.

Mbali na kuwasaidia raia wa Zambia kupata chakula wakati huu wa uhitaji, pamoja na kuimarisha uhusiano, udugu na ushirikiano baina ya nchi hizi, makubaliano hayo yanayotekelezwa kwa kipindi cha miezi nane yataiingizia Tanzania TZS bilioni 650.

Zaidi ya hekari milioni 1 ziliathiriwa na ukame nchini Zambia pamoja na mvua za El Nino na hivyo kuiweka nchi hiyo katika uhitaji mkubwa wa chakula ili kunusuru maisha ya wananchi wake.

Tanzania na Zambia ni marafiki wa muda mrefu katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika ambapo ushirikiano wao ulianza tangu wakati wa kupigania uhuru chini ya waasisi wa mataifa haya Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Kenneth Kaunda. Udugu huu wa miaka na mikaka unathibitishwa na miradi ya uwili kama Boma la Mafuta la Tanzania na Zambia (TAZAMA) pamoja na Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).

Waziri Makamba ashiriki mkutano wa 45 wa Baraza la Mawaziri wa EAC

Tanzania inaiuzia Zambia mahindi tani 650,000 kukabiliana na njaa