in , ,

Waziri Makamba ashiriki mkutano wa 45 wa Baraza la Mawaziri wa EAC

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba (Mb.) ameongoza ujumbe wa Tanzania kushiriki Mkutano wa Kawaida wa 45 wa Baraza la Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) uliofanyika tarehe 28 Juni, 2024 jijini Arusha.

Mkutano huu pamoja na masuala mengine umepitia na kujadili masuala mbalimbali ya kipaumbele katika ukanda wa EAC ambayo ni, Maendeleo ya Miundombinu, forodha na biashara, masuala ya siasa na kijamii, taarifa ya kamati ya rasilimali watu pamoja na kupokea taarifa ya kamati ya ukaguzi na udhibiti wa hesabu za jumuiya kwa kipindi cha mwaka wa fedha unaoishia Juni 2023.

Masuala mengine ni pamoja na, jitihada za kubidhaisha Kiswahili kikanda na kimataifa sambamba na taarifa ya Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani tarehe 7Julai ambayo kikanda yatafanyika nchini Kenya na kuhudhuriwa na Nchi wanachama za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Kadhalika, mkutano huu pia umejadili na kusisitiza umuhimu wa kuwasilisha michango ya mwaka kwa wakati kutoka kwa nchi zote wanachama ili kuiwezesha Sekretarieti ya EAC kujiendesha na kutekeleza kwa ufanisi majukumu yake ya kikanda.

Aidha, kupitia mkutano huo Katibu Mkuu Mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Veronica Mueni Nduva alijitambulisha kwa Baraza hilo na kueleza nia yake ya kusimamia ustawi wa kikanda katika kukuza uchumi, uvumbuzi, biashara, ajira na amani na usalama kwa maendeleo endelevu ya wananchi wa EAC.

Viongozi wengine wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na, Naibu Waziri Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki – anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Stephen Byabato (Mb.), Naibu Waziri, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Stanslaus Nyongo (Mb.), Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.

Mkutano huo umefanyika chini ya Uenyekiti wa Jamhuri ya Sudan Kusini na umehudhuriwa na Nchi zote Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, isipokuwa Somalia imeshiriki kwa njia ya mtandao.

Tabora United hatarini kufungiwa uwanja wa nyumbani kwa kuvunja kanuni za ligi

Tanzania inaiuzia Zambia mahindi tani 650,000 kukabiliana na njaa