Balozi wa Tanzania awasilisha Hati za Utambulisho Vatican
Balozi wa Tanzania awasilisha hati za utambulisho Vatican Balozi Hassani Mwamweta amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Baba Mtakatifu Francis nchini Vatican Juni 8, 2024, hatua inayompa uhalali wa kutekeleza majukumu yake kama Balozi wa Tanzania kwenye Ukulu Mtakatifu ( Holy See).
Hafla ya uwasilishaji wa nyaraka hizo umehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Vatican akiwemo Mwadhama Pietro Kadinali Parolin mwenye wadhifa wa Waziri Mkuu, pamoja na Askofu Mkuu, Paul Gallagher, Waziri wa Mambo ya Nje wa Vatican.
Balozi Mwamweta ambaye makazi yake ni Berlin, Ujerumani pia anaiwakilisha Tanzania kwenye mataifa mengine sita ambayo ni Poland, Uswisi, Hungary, Jamhuri ya Czech, Bulgaria, Slovakia na Romania.
Kwa muda mrefu Vatican kupitia Kanisa Takatifu Katoliki imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali nchini Tanzania yenye kugusa sekta mbalimbali, zaidi sana ikiwa ni sekta ya afya na elimu.
Ikumbukwe kuwa hii ni ishara ya matokeo mazuri ya ziara ya kikazi ya Rais Samia Suluhu Hassan nchini Vatican Februari 11 hadi13, 2024 iliyolenga kudumisha ushirikiano mzuri wa kihistoria baina ya Tanzania na Vatican.