50 wakamatwa kwa kuvamia ofisi na kuwajeruhi maafisa wa Msitu

Jeshi la Polisi mkoani Geita linawashikilia watuhumiwa hamsini kwa tuhuma za kuvamia ofisi ya Hifadhi ya Msitu wa Lwamgasa iliyopo Kijiji cha Lwamgasa wilayani Geita kwa tuhuma za kuwashambulia na kuwajeruhi maafisa wa Msitu wanne pamoja na kuharibu mali mbalimbali za ofisi.
Taarifa ya Polisi imesema chanzo cha tukio hilo lililotokea Agosti 13, 2025, ni kundi la wahalifu hao kujichukulia sheria mkononi kwa kuwazuia maafisa hao wasitekeleze majukumu yao, wakishinikiza maafisa hao waache wazi maeneo ya hifadhi yasipandwe miti ili wayatumie kwa shughuli za kilimo.
“Jeshi la Polisi linaendelea kuwahoji watuhumiwa hao na upelelezi utakapokamilika watafikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria, ” imesema taarifa hiyo.
Jeshi la Polisi limetoa onyo kali kwa wananchi kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi na halitasita kuchukua hatua kali za kisheria.







