Serikali imepanga kutumia kiasi cha shilingi trilioni 34.88 katika mwaka wa fedha 2020/2021 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo ikiwa ni ongezeko la shilingi trilioni 1.76 kulinganisha na bajeti ya mwaka 2019/2020 ya shilingi trilioni 33.11.
Hayo yamesemwa Leo jijini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango wakati akitoa tathmini ya utekelyezaji wa Mpango wa mwaka 2019/20 na mapendekezo ya Mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2020/21
Dkt. Mpango ameeleza kuwa kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 21.98 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi trilioni 12.90 ni za matumizi ya maendeleo, ambazo ni sawa na asilimia 37 ya bajeti yote.
“Bajeti ya maendeleo inajumuisha shilingi trilioni 10.16 fedha za ndani, sawa na asilimia 78.8 ya bajeti ya maendeleo na shilingi trilioni 2.74 fedha za nje, matumizi haya yanajumuisha gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu wa 2020”
Waziri Mpango, aliongeza kuwa mpango na bajeti kwa mwaka 2020/21 unazingatia azma ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa viwanda na kuboresha ustawi wa jamii.
Aidha, alisema kuwa bajeti hii itaendelea na utekelezaji wa maeneo makuu manne ambayo ni kuondoa umasikini, kupunguza ukosefu wa ajira kwa vijana, kuendeleza vita dhidi ya rushwa na ubadhirifu wa mali za umma, pamoja na kuendelea kudumisha amani, ulinzi na usalama wa maisha ya wananchi na mali zao.
Ili kufikia malengo hayo, Serikali itaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani, kugharamia shughuli za Serikali ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati na uboreshaji wa huduma za kijamii kwa lengo la kuleta maendeleo kwa haraka.