TANESCO haihitaji ruzuku ya serikali na litaanza kutoa gawio- Waziri Dk Kalemani

0
26

Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani amesema kwamba Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa sasa halihitaji ruzuku kutoka serikalini na kuanzia mwaka ujao wa fedha, 2019/20 litaanza kutoa gawio (serikalini).

Dk Kalemani aliyesema hayo jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha bajeti ya wizara yake ambapo alibainisha kuwa Tanesco kwa sasa haihitaji ruzuku ya Serikali katika shughuli zake za uendeshaji kutokana na kujiendesha lenyewe na kuokoa wastani wa Sh143 bilioni zilizokuwa zikitumika kama ruzuku kutoka serikalini kila mwaka.

Mapato ya TANESCO yameimarika kwa kiwango cha ongezeko la asilimia 1.5 mwaka 2017/18 hadi asilimia 7.6 mwaka 2018/19. Hivyo ni matarajio kuwa shirika hilo litaweza kuanza kutoa gawio serikalini katika kipindi cha mwaka 2019/20, alisema Dk Kalemani.

Alisema TANESCO imeunganishia umeme kwa wateja wapya 969,431 katika kipindi cha kuanzia Julai 2015 hadi Mei 15, 2019 na kufikia wateja 2,442,648 ikilinganishwa na wateja 1,473,217 waliokuwepo kuanzia nchi ilipopata uhuru hadi Juni, 2015 sawa na ongezeko la asilimia 66 kwa miaka mitatu.

Aidha, katika kuhakikisha ufanisi wa shirika hilo, Dk Kalemani alisema kuwa wameanzisha utaratibu mpya wa mawasiliano baina ya wateja na Tanesco kupitia mitandao ya kijamii ikiwemo kuanzisha makundi ya WhatsApp kwa kila wilaya yanayopatikana saa 24 ili  kuimarisha huduma kwa wateja, kuongeza ufanisi na mapato ya shirika hilo.

Send this to a friend