Serikali yaeleza sababu ya kuiwekea 'kikwazo' mizigo inayoingia kutoka Zanzibar

0
24

Serikali imetolea ufafanuzi kuhusu kitendo cha mizigo inayoingizwa kutoka Zanzibar kuja Tanzania Bara kuwekewa vikwazo, sawa na mizigo nayoingizwa kutoka nchi nyingine, ambapo imesema kuwa ni kutokana na mifumo tofauti ya uthaminishaji wa mizigo inayotumiwa katika pande hizo mbili za muungano.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Fedha, Dk Ashatu Kijaji amesema kuwa, Mamlaka ya Mapato Tanzania Bara ya Mamlaka ya Mapato Zanzibar zinatumia mifumo tofauti katika uthaminishaji wa mizigo, ndio sababu mizigo inayoingia kutoka Zanzibar hulazimika kuthaminishwa tena.

Ametoa ufafanuzi alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji aliyetaka kujua kwanini wageni wanapotaka kuingia na magari yao Tanzania Bara kwa ajili ya matumizi binafsi hupewa vibali kwenye mipaka ya nchi, lakini wananchi wanaotaka kuingia na magari yao kutoka Zanzibar na kuyatumia kisha kuondoka nao huwekewa vikwazo.

Dk Kijaji aliendelea kutoa ufafanuzi huo akisema kuwa, kutokana na utofauti huo wa mfumo wa uthaminishaji, hivyo TRA inalazimika kuthaminisha upya mizigo yakiwemo magari yanayoingia kutoka Zanzibar ili kujiridhisha na kodi iliyolipwa katika hali ya kutengeneza mazingira yenye ushindani sawa ya biashara.

Aidha alisema jambo hilo linafahamika huku akiwasihi wabunge kutoka Zanzibar kufikia muafaka wa jambo hilo, ili serikali iweze kuwahudumia wananchi pasi na kuwa na mkanganyiko wowote.

Send this to a friend