Corona: Marekani yasitisha ufadhili kwa Shirika la Afya Duniani (WHO)

0
28

Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa amewaagiza maafisa wa serikali kusitisha ufadhili wa nchi hiyo kwa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Akizungumza na waandishi wa habari, Rais Trump amesema kuwa WHO imeshindwa kutekeleza majukumu yake ya msingi katika mapambano dhidi mlipuko wa virusi vya Corona.

Amelituhumu shirika hilo la Umoja wa Mataifa (UN) kwa kuwa na uongozi mbaya, na kutokuwa na uwazi kuhusiana na kusambaa kwa virusi hivyo vilivyoanzia nchini China, na kwamba WHO inapaswa kuwajibishwa.

Awali amewahi kunukuliwa akilituhumu shirika hilo kuwa upande wa China katika vita dhidi ya corona.

Hata hivyo kiongozi huyo amekosolewa vikali kutokana na namna ambavyo serikali yake inakabiliana na janga hilo la dunia ambapo hadi Aprili 14, 2020, zaidi ya watu 26,000 wamefariki nchini humo. Marekani ndiyo nchi iliyoathiriwa zaidi na mlipuko wa virusi vya corona.

Akizungumzia uamuzi huo, Katibu Mkuu wa UN, António Guterres amesema huu sio wakati wa kukatisha ufadhili kwa shirika hilo linaloongoza mapambano dhidi ya COVID-19.

Marekani ndiyo nchi inayotoa mchango mkubwa wa kifedha kwa WHO ambapo mwaka 2019 ilichangia TZS 925 bilioni, ambayo ni pungufu kwa asilimia 15 kufikia lengo lake.

Kwa upande wa China, katika mwaka 2018/19 ililichangia shirika hilo jumla yaa TZS 199 bilioni.

Send this to a friend