Serikali imewahakikishia Watanzania kuwa hakuna upungufu wa sukari hivyo hawapaswi kuwa na wasiwasi wa aina yoyote ile.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akitoa ufafanuzi juu ya malalamiko ya wananchi kuhusu kupanda kwa bei ya sukari.
Bashungwa amesema ni kweli bei ya sukari imepanda lakini haisababishwi na upungufu wa sukari bali imesababishwa na waagizaji kushindwa kuagiza kwa wakati kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu unayosababishwa na kirusi cha Corona.
Ili kukabiliana na kadhia hiyo serikali imetoa vibali vya jumla ya tani 40,000 kwa kampuni nne za wazalishaji ambapo kila kampuni imeagiza tani 10,000.
Waziri Bashungwa amesema kuwa tayari sukari iliyokwisha ingia bandarini kupitia kampuni ya Kagera Sugar ni tani 9,990 na imeanza kutolea bandarini tangu jana jioni.
Kadhalika amesema hadi Mei 30 mwaka huu, kampuni mbalimbali zinazofanya biashara ya kuingiza sukari nchini zitakuwa zimeingiza tani 30,200 kwa ajili ya matumizi.
Katika hatua nyingine Waziri Bashungwa amesema kuwa wizara inatarajia kuomba nyongeza ya tani 58,000 ili kukidhi mahitaji ya sukari kufikia Juni 2020