Na Mwanaheri Khamis, Unguja 17.04.2020
Tangu nchi za bara Afrika kuanza kutangaza visa vya wagonjwa wa kirusi cha homa ya corona, shughuli za biashara zimeathirika kwa namna mbalimbali barani hapa.
Kama ilivyo kwa nchi nyingi duniani, Tanzania nayo inapata changamoto hii. Katika miaka ya karibuni, Tanzani imeingia kwa nguvu zote kuhakikisha inabadilika kuwa nchi ya viwanda yenye uchumi wa kati kufikia mwaka 2025. Kufikia hilo kila juhudi inawekwa katika kujenga uchumi wa taifa, wenye biashara na viwanda mbalimbali.
Huku Tanzania ikiendelea na nia yake hiyo kufikia lengo lake COVID-19 imekuwa changamoto kwenye kasi ya kukua mfano kwenye eneo kama utalii ambapo mwezi Machi mwaka huu baadhi ya hoteli zilisitisha huduma zake kwa muda huku Waziri wa Utalii akionyesha video kwamba japo kuna changamoto lakini anatumaini tutarejea tena baada ya janga hili kupita na kuendelea.
Katika hatua nyingine, juma hili Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametangaza kuahirisha sherehe za Mei Mosi ambazo hufanyika Mei 1 kila mwaka. Waziri Mkuu kaongeza pia kuwa mikusanyiko isiyo lazima isitishwe na kutaka watu kukaa nyumbani kama hakuna jambo ambalo ni muhimu kuwafanya kutoka nje.
Biashara nyingi nazo zimechukua hatua kupunguza kukutana uso kwa uso wengi wakitaka wafanyakazi kufanya majukumu yao kutokea nyumbani au kuahirisha shughuli ambazo zinahitaji watendaji kukutana.
Aina hii ya maisha itatawala biashara na shughuli zetu nyingi sasa na siku zijazo wakati tunapigana na kirusi huyu. Naiwaza kwa mfano shughuli ya kampuni ya Tigo Tanzania kuweka hisa zake sokoni (IPO) katika soko la hisa la Dar es Salaam (DSE).
Mchakato wa kuingiza kampuni katika soko la hisa ni shughuli ya kuleta watu pamoja, mikutano, majadiliano na safari hasa za nje ya nchi ambazo zimesitishwa. Je shughuli kama hizi ziendelee? Busara yaweza kuwa kuahirisha shughuli kama hizi na kukusanya nguvu pamoja kupigana na kirusi huyu kwanza kisha kurejea tukiwa salama na utulivu hili likishapita.