Wasifu wa mwendazake Askofu Getrude Rwakatare
Taarifa katika Wasifu huu ni kwa mujibu wa Tovuti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Jina lake ni Getrude Pangalile Rwakatare, alizaliwa Disemba 31, 1950, na amefariki akiwa na umri wa miaka 69.
ELIMU
Alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Mbingu na Shule ya Msingi ya Wasichana Ifakara kuanzia mwaka 1957 hadi 1960 na 1961 hadi 1964 mtawalia.
Baada ya hapo mwaka 1965 hadi 1968 alipata elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Korogwe, mkoani Tanga, na mwaka 1971 alijiunga Chuo cha Railways ambapo alihitimu ngazi ya astashahada mwaka 1972.
Mwaka 1974 hadi mwaka 1975 aipata elimu katika ngazi ya stashahada kutoka North London Polytechnic. Alijiunga na Mood Bible Institute cha Chicago nchini Marekani mwaka 1984 ambapo alihitimu Shahada (ya kwanza) ya Sanaa katika Theolojia mwaka 1988.
KAZI
Dkt. Rwakatare amefanya kazi sehemu mbalimbali ambazoni ni pamoja na:
Meneja Wafanyakazi wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (1970-1983)
Mwenyekiti wa Pan African Christian Women Assembly (1989-1993)
Mchungaji wa Kanisa la Mlima wa Moto (1995-2017)
Mkurugenzi wa St. Mary’s International School (1996-2017)
Mkurugenzi wa St. Mary’s Teachers College (2003-2017)
Mtangazaji Mlima wa Moto (2004-2017)
SIASA
Mwaka 2005 alikuwa Mlezi wa Wanawake wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ngazi ya wilaya nafasi aliyoitumikia kwa mwaka mmoja. Aliteuliwa kuwa Mbunge wa Viti Maalum kupitia CCM mwaka 2007, nafasi aliyoitumikia hadi 2015.
Katika kipindi cha hicho (2007-2010) akiwa bungeni alikuwa mjumbe wa kamati ya maendeleo ya jamii, na kati ya mwaka 2010-2015 alikuwa mjumbe wa kamati ya huduma za jamii.
Aidha, mwaka 2017 aliteuliwa tena kuwa mbunge wa viti maalum kupitia chama hicho nafasi aliyokuwa akiitumikia hadi mauti yalipomkuta Aprili 20, 2020.
Chanzo: Bunge la Tanzania (https://www.parliament.go.tz/administrations/572)