Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kesho Aprili 22, 2020 anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika maombi maalum ya kuliombea taifa dhidi ya maambukizi ya homa kali ya mapafu (COVID-19) inayosababishwa na virusi vya corona.
Maombi hayo yameandaliwa na wizara ya afya kwa kushirikiana na viongozi wa madhehebu ya dini nchini, na yatafanyika katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi.
Wizara imeeleza kuwa viongozi wachache watahudhuria hafla hiyo kuwawakilisha wananchi ikiwa ni hali ya kuchukua tahadhari ya maambukizi ya virusi hivyo, huku wananchi wakisisitizwa kufuatilia maombi kupitia vyombo vya habari.
Maombi hayo ni utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa viongozi wa dini na serikali uliofanyika Aprili 9 mwaka huu, na pia ni mwendelezo wa siku tatu za maombi zlizotangazwa na Rais Dkt. John Magufuli kuanzia Aprili 17-19, 2020.