Taarifa ya serikali kuhusu mtihani wa kidato cha sita 2020
Wizara ya elimu nchini Tanzania imeahirisha mtihani wa kidato cha sita mwaka 2020 hadi hapo itakapoamuliwa vinginevyo kutokana na janga la virusi vya corona lililoikumba dunia.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dkt. Leonard Akwilapo wakati akijibu maswali kutoka kwa wazazi na wanafunzi wa kidato cha sita waliotaka kujua hatma yao baada ya serikali kufunga shule zote.
“Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) limesambaza barua kwa makatibu tawala wa mikoa na wilaya zote na katika shule za umma na binafsi kuwataarifu kuhusu kusitishwa kwa mitihani hiyo hadi serikali itakapotangaza vinginevyo,” amesema Akwilapo.
Kauli hiyo imekuja kufuatia wanafunzi na wazazi kuwa na maswali mengi endapo mitihani hiyo iliyopangwa kuanza Mei 04 mwaka huu, ingeanza kama ratiba inavyoonesha au la.
Licha ya mitihani kutokuwepo kama ilivyopangwa, wizara imewasihi wanafunzi kuendelea kujisomea muda wote wawapo majumbani.
Mapema Machi mwaka huu Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitangaza kufunga shule zote ikiwa ni miongoni mwa mikakati iliyochukuliwa na serikali kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona