Serikali kupitia Wizara ya Afya imeeleza kuwa kwa muda wa siku saba sasa haijatoa taarifa za hali ya maambukizi ya virusi vya corona nchini kwa sababu kuna maabara ya taifa ipo katika matengenezo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu wakati akizindua mfumo wa mawasiliano wa huduma kwa wateja katika wizara hiyo ambapo amebainisha kuwa taarifa zitatolewa baada ya matengenezo hayo kukamilika hivi karibuni.
Amesema kuwa licha ya kuwa taarifa hazitolewi, lakini ugonjwa wa corona bado upo, hivyo amewataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wanapotekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Ugonjwa huu [COVID-19] tutaendelea kuwa nao kwa miezi kadhaa, hivyo inatupasa kujifunza kuishi nao huku tukichukua tahadhari ya kujikinga kama yalivyo magonjwa mengine ya kuambukiza,” amesema Ummy.
Amewasihi wananchi kuondoa hofu na kwamba kitu cha muhimu ni kuchukua tahadhari.