Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu amesema kuwa kuna haja ya Watanzania kujifunza kuishi na virusi vya corona kwa sababu vitaendelea kuwepo kwa miezi kadhaa.
Ummy Mwalimu amesema hayo wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo watoa huduma 600 wa ngazi ya jamii katika kufanya ufuatiliaji wa tetesi za wagonjwa wa homa ya mapafu (COVID-19) na watu wanaokaa karibu na wagonjwa hao.
“Corona itaendelea kuwepo kwa miezi kadhaa, ni lazima tujifunze kuishi na corona, ni lazima maisha yaendelee,” amesema waziri huyo.
Hata hivyo amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na ugonjwa huo wanapoendelea na shughuli zao za kila siku.
Watoa huduma hao mbali na kufuatilia tetesi za wagonjwa pia watatumika kutoa ushauri jinsi ya kujikinga, na kutoa taarifa sahihi za ugonjwa huo. Kwa Jiji la Dar es Salaam, Ummy Mwalimu amesema kila mtaa angalau utakuwa na mtoa huduma mmoja ngazi ya jamii.