Tanzania na Rwanda zimefikia makubaliano juu ya mpango mkakati wa kusafirisha mizigo baina ya nchi hizo mbili katika kipindi hiki cha janga la virusi vya corona.
Makubaliano hayo yamefikiwa kufuatia mkutano uliofanyika Mei 15 mwaka huu kati ya maafisa baina ya nchi hizo kwa njia ya video.
Makubaliano yaliyofikiwa ni, kwanza, kusitisha mara moja mpango wa kubadilishana madereva katika Mpaka wa Rusumo.
Pili, mizigo inayosafirishwa kwenda Rwanda itashushwa mpaka, isipokuwa kwa malori yaliyobeba vitu vya kuharibika na mafuta ambayo yataruhusiwa kuingia nchini humo kati ya saa 12 alfajiri hadi saa 12 jioni na yatasindikizwa hadi yanapokwenda.
Tatu, nchi hizo zimekubaliana kuwa madereva wanaokwenda Rwanda watalala katika eneo lililotengwa kwa gharama zao.
Nne, nchi hizo zimekubaliana kuwa kuwapima madereva virusi vya corona itakuwa lazima, na upimaji utaratibiwa na serikali ya Tanzania katika maeneo ambayo madereva waanzia safari. Pia, kutokana na umbali kati ya Rusumo na Dar es Salaam, madereva watapimwa njiani katika vituo vilivotengwa.
Rwanda imesema itahakikisha uwepo wa vifaa vya kupima kwa madereva wanaosafirisha magari pamoja na bidhaa za kuharibika na mafuta.
Tano, nchi hizo mbili zimekubaliana kuwa zitawasiliana kwanza kabla ya kutekeleza mpango mpya wa kiafya wa kiakabiliana na COVID-19 ambao unaweza kuathiri biashara za mipakani.