Corona: Kenya yakana kuzuia madereva wote wa Tanzania

0
27

Serikali ya Kenya imesema kuwa haijafunga mpaka wake kwa sababu ya Tanzania bali imefunga kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Pia, nchi hiyo ya Afrika Mashariki imekanusha taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari kuwa imewazui madereva wote wa Tanzania wanaoendesha malori ya mizigo kuingia nchini humo.

Hayo yamesema na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dan Kazungu alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 19, 2020 jijini Dar es Salaam, ambapo ameeleza kuwa, vyombo vya habari havikuandika kila kitu ambacho Rais wa Kenya alisema.

“Aliposema kuhusu agizo la mpakani alisema Mtanzania anayepimwa na akawa negative [hana maambukizi] aingie kwenye gari apeleke mzigo wake Kenya. Hili watu hawaongei,” amesema Kazungu.

Aidha, amesema utaratibu huo huo umewekwa nchini Kenya kwamba dereva hatoruhusiwa kutoka kwenda Tanzania au Uganda bila kupimwa na kudhibitika kuwa hana maambukizi, ili asije akawaambukiza wengine huko aendako.

Akitumia msemo wa Kiswahili “Vita vya panzi furaha wa kunguru” amesema ifahamike kuwa katika haya yote kunguru ni kirusi cha corona hivyo Tanzania na Kenya zikiendelea kuzozana, kirusi kitawadonoa wote.

Kauli ya balozi huyo imekuja siku moja baada ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Martin Shigella kuliagiza jeshi la polisi kuhakikisha kuwa magari kutoka Kenya hayapiti katika Mpaka wa Horohoro kuingia Tanzania.

Send this to a friend