Marekani yaipa Tanzania bilioni 5 kupambana na corona

0
23

Marekani imetangaza kuipatia Tanzania nyongeza ya $2.4 milioni (TZS 5.6 bilioni) kwa ajili ya kuwezesha mapambano dhidi ya maambukizi ya homa ya mapafu (COVID-19) inayosababishwa na virusi vya corona.

Fedha hizo ambazo zinatolewa kupitia Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) zitaelekezwa katika masuala mbalimbali yakiwamo kuimarisha maabara, mawasiliano, maji na vitakatishi, kupambana na kudhibiti maambukizi, pamoja na kutoa elimu kwa umma.

Taarifa iliyotolewa na ubalozi wa nchi hiyo Tanzania inaeleza kuwa fedha hizo ni sehemu ya ahadi ya $3.4 milioni (TZS 7.9 bilioni) ambazo nchini hiyo ilitangaza kutoa kwa ajili ya janga la corona, ambapo katika awamu ya kwanza ilitoa $1 milioni (TZS 2.3 bilioni).

Aidha, Marekani imeelekeza kiasi kingine cha $1.9 milioni (TZS 4.4 bilioni), na hivyo kufanya jumla ya fedha ilizoipa Tanzania kukabiliana na COVID-19 kufikia $5.3 milioni (TZS 12.2 bilioni), taarifa hiyo imeeleza.

Katika kipindi cha miaka 20 iliyopita Marekani imewekeza $7.5 bilioni (TZS 17.3 trilioni) nchini Tanzania, ambapo kati ya fedha hizo, $4.9 bilioni (TZS 11.3 trilioni) zimeelekezwa kwenye sekta ya afya.

Send this to a friend