Corona: Raia wa kigeni 482 waondoka nchini Tanzania

0
24

Kufuatia serikali ya Tanzania kuruhusu kutua nchini kwa ndege zinazokuja kuwachukua raia wa kigeni waliokuwa wamekwama nchini kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa homa ya mapafu (Covid-19), jumla ya raia wa kigeni 482 wameondoka nchini.

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaeleza kuwa raia walioondoka ni 133 wa Uturuki, 260 wa Visiwa vya Comoros na 89 wa Uingereza.

Aidha, Tanzania imefanikiwa kuwarejesha nchini Watanzania 300 waliokuwa wamekwama kwenye nchi mbalimbali kutokana na mlipuko wa virusi vya corona uliopelekea nchi nyingi kusitisha huduma ya safari za anga.

Watanzania waliorejeshwa nchini wametoka India, Uturuki, Misri, Visiwa vya Comoros na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Wizara imesema kuwa zoezi la kuwarejesha nchini Watanzania waliokwama kwenye nchi mbalimbali ni endelevu, na kwamba wenye nia ya kurejea wajiandikishe katika balozi za Tanzania kwenye nchi walizomo ili utaratibu wa kuwasafirisha uandaliwe.

Send this to a friend