Uchunguzi Maabara ya Taifa: Mashine moja ya kupima corona ilikuwa na hitilafu
Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto amesema kuwa mashine moja ya kupima sampuli za ugonjwa wa homa ya mapafu (Covid-19) katika Maabara ya Taifa ya Afya ja Jamii ilikuwa na hitilafu.
Ummy Mwalimu amesema hayo ikiwa ni sehemu ya ripoti ya uchunguzi wa maabara hiyo, ambapo ameongeza kuwa, licha ya mashine hiyo kuwa na hitilafu kwa takribani miezi miwili, uongozi wa maabara haukuchukua hatua za kuifanyia matengenezo kwa wakati.
Aidha, Waziri Ummy amesema kamati ya uchunguzi imebaini kuwepo mapungufu katika mfumo wa kimuundo, kiutendaji, na uendeshaji wa kitaaluma katika upimaji wa vipimo, uhakiki wa ubora wa majibu na udhaifu katika uhifadhi wa vipimo vya Covid-19.
Pia, imebainika kuwepo kwa upungufu wa wataalamu wenye sifa za mafunzo ya biotechnology na molecular biology katika sekta ya afya na katika maabara ya taifa.
Majibu hayo yamekuja ikiwa ni siku 20 tangu Rais Dkt Magufuli alipoagiza maabara hiyo kuchunguzwa kuhusu mchakato mzima wa upimaji wa corona, baada ya sampuli zisizo za binadamu kutajwa kuwa zina maambukizi.
Katika hatua nyingine waziri amesema kuwa upimaji wa Sampuli zote za Covid-19 umehamishiwa katika maabara mpya iliyokamilika kujengwa katika eneo la Mabibo jijini Dar es Salaam ambayo kwa sasa ndiyo itakuwa Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii.
Amesema maabara hiyo mpya ina uwezo wa kupima sampuli 1,800 za ugonjwa wa Covid -19 ndani ya masaa 24 tofauti na ile ya awali iliyokua na uwezo wa kupima sampuli 300 tu.