Polisi waingilia sakata la mwanamke anayeidaiwa kufumaniwa na mume wa mtu
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limeanza kufanya uchunguzi kuhusu tukio la Vena Mushi kupigwa kwa madai ya kufumaniwa na mume wa mtu.
Akizungumza baada ya kumtembelea hospitalini, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kuwa Vena ameumia sana na anahitaji uangalizi wa karibu.
“Jana nilifanikiwa kwenda kumtembelea yule mwanamke aliyedaiwa kufumaniwa na mume wa mtu hapa mkoani Kilimanjaro na kumjulia hali. Ameumia na anahitaji uangalizi sahihi wa afya yake. Polisi wameanza uchunguzi ninaamini atapata haki yake,” ameandika Mgwira kupitia ukurasa wake wa Twitter.
Hivi karibuni video zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikionesha Vena ambaye ni Mkazi wa Kata ya Msaranga katika Manispaa ya Moshi akipigwa na mwanamke mwingine ambaye alijitambulisha kuwa mke halali wa mume aliyefumaniwa.
Katika video hizo, Vena anasikika akisema kuwa hakuwa anafahamu kama mwanaume huyo alikuwa na mke, na endapo angefahamu, asingekubali kuwa naye.
Pia, amedai kuwa fedha zake TZS 900,000 zilichukuliwa na mwanamke huyo aliyekuwa akimpiga. Amesema fedha hizo zilikuwa ni za biashara aliyokuwa amepanga kushirikiana na mwanaume anayedaiwa kufumaniwa naye.