WHO: Sababu kuu mbili za Afrika kuepuka athari kubwa za corona

0
12

Mei 25, 2020 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Afrika, ambapo ilitimia miaka 57 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (AU), Shirika la Afya Duniani (WHO) lililipongeza bara hilo kwa namna lilivyokabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.

Licha ya kusema kuwa huenda kuna visa havijarekodiwa, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus ameipongeza Afrika kwa kuwa na 1.5% ya visa vyote vilivyoripotiwa duniani, na chini ya 0.1% ya vifo. Matokeo hayo yanaonesha kuwa Afrika ndio ukanda ulioathiriwa kwa kiwango kidogo zaidi na janga hilo.

Kikubwa kilichojificha nyuma ya mafanikio ya Afrika katika janga hili kinatajwa kuwa ni nchi nyingi za Afrika kuwa na uzoefu wa kupambana na magonjwa yanayoambukiza kama vile polio, surua, ebola, homa ya manjano, mafua, na mengine mengi, amesema Tedros.

Aidha, sababu nyingine zimetajwa kuwa ni nchi nyingi za Afrika kujiandaa mapema kukabiliana na ugonjwa wa homa ya mapafu (Covid-19), licha ya gharama kubwa kwa wananchi na uchumi.

Baadhi ya wataalamu wametahadharisha kuhusu uwepo wa janga la kimya kimya (silent pandemic), huku wakisisitiza uwepo wa taarifa na takwimu za mara kwa mara kuhusu mwenendo wa virusi vya corona.

Viongozi wa Afrika wameshauriwa kuhakikisha wanawapima watu, wanawafuatilia waliokuwa karibu na wenye maambukizi, kufanya tafiti kwa ajili ya chanjo, na wasiruhusu sekta ya afya ielemewe.