Serikali yaruhusu mashabiki viwanjani, yaweka masharti

0
22

Siku moja kabla ya kufikia Juni Mosi 2020, ambayo ndiyo siku shughuli za michezo zitarejea rasmi nchini baada ya kuzuiwa kwa zaidi ya miezi miwili, serikali imesema kuwa ni ruksa kwa mashabiki kwenda viwanjani.

Hayo yemesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi ambapo ameongeza kuwa mashabiki wataruhusiwa katika michezo yote, isipokuwa ile ambayo itajaza uwanja, na kupelekea mashabiki kusongana.

Amesema mashabiki wawapo viwanjani wanatakiwa kukaa kwa umbali wa mita moja kutoka shabiki mmoja hadi mwingine, kuepuka misongamano wakatiwa kuingia na kutoka viwanjani, kuvaa barakoa, kunawa mikono kwa sabuni na maji tiririka au kutumia vipukusi (sanitizers) kabla ya kuingia viwanjani.

Dkt. Abbasi ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali ameonya kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wataokaidi maelekezo hayo.

Ligi Kuu ya Mpira wa Miguu Tanzania Bara inatarajiwa kuanza kutimu vumbi Juni 13 mwaka huu, ikiwa ni takribani miezi mitatu tangu ilipozuiwa Machi 2020, ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.

Send this to a friend