Magari 11 ya anasa ya Makamu wa Rais wa Equatorial Guinea kupigwa mnada

0
10

Magari ya anasa (luxury) ya Makamu wa Rais wa Equatorial Guinea, Teodoro Nguema Obiang Mangue yataigwa mnada Septemba 29 mwaka huu na mamlaka nchini Uswisi.

Magari hayo 11 ya Teodoro ambaye mbali na kuwa Makamu wa Rais pia ni mtoto wa Rais wa taifa hilo la Afrika ya Kati, Teodoro Obiang Nguema Mbasogo, yanakadiriwa kuwa na thamani ya TZS 30 bilioni.

Magari hayo yalikamatwa mwaka 2016 ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa mashtaka ya rushwa na utakatishaji fedha yaliyokuwa yakimkabili kiongozi huyo maarufu kwa kuishi maisha ya anasa.

Miongoni mwa magari yatakayouzwa katika mnada huo ulioandaliwa na kampuni ya udalali kutoka London, Uingereza ni Lamborghini Veneno, LaFerrari, Koenigsegg One:1 (magari haya yalitengenezwa 7 pekee duniani), McLaren P1, Aston Martin One-77 na Bugatti Veyron.

Polisi jijini Geneva walikamata magari hayo katika eneo la mizigo katika uwanja wa ndege jijini humo baada ya kufunguliwa kesi dhidi ya kiongozi huyo.

Teodoro amewahi kuilipa mamlaka nchini Marekani TZS 689 bilioni ili kumaliza kesi iliyokuwa ikimkabli ya kutumia mali zilizoibwa katika nchi yake kujipatia vitu mbalimbali vya anasa kama vile jumbe la kifahari lililopo California, ndege binafsi, na galvu (glove) aliyovaa nguli wa muziki, Michael Jackson katika moja ya matamasha yake.

Mwaka jana vyombo vya habari nchini Brazil viliripoti kuwa mamlaka nchini humo zilikamata fedha taslimu TZS 37 bilioni na saa za anasa katika msafara wa kiongozi huyo.

Baba yake alitwaa madaraka kwa mapinduzi ya kijeshi mwaka 1979, na alimteua mwanae kuwa kushika wadhifa huo mwaka 2016.

Send this to a friend