Wakati Bunge la 11 likielekea ukingoni tayari kwa maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson ameweka wazi kuwa atagombea katika uchaguzi huo.
Dkt. Tulia ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma katika mkutano wa 19, kikao cha 46 alipopewa nafasi ya kuzungumza ambapo pamoja na kuweka wazi kusudio la kugombea, pia ameipongeza serikali kwa hatua mbalimbali ilizochukua kuhakikisha inawaletea wananchi maendeleo.
“Nami nimepata hamasa ya kujitosa. Na Inshallah Mwenyenzi Mungu atujalie uzima na afya, yumkini nitakwenda mahali fulani, kuomba ridhaa ya wananchi wenzangu ya kuwatumikia katika bunge lako [Spika wa Bunge] tukufu,” amesema Tulia.
Aidha, kiongozi huyo hajaweka wazi atagombea jimbo gani, lakini kumekuwapo tetesi kuwa huenda akagombea katika Jimbo la Mbeya Mjini ambalo sasa linaongozwa na Mbunge Joseph Mbili kupitia CHADEMA.
Novemba 2015 baada ya kuingia madarakani, Rais Dkt. Magufuli alimteua Dkt. Tulia kuwa mbunge ambapo kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alichaguliwa kuwa Naibu Spika wa Bunge la 11 la Tanzania kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) baada ya kumshinda mpinzani wake kutoka Chama cha Wananchi (CUF) Mhe. Magdalena Sakaya.