Mfumuko wa Bei wa Taifa waongezeka hadi asilimia 3.7 kutoka asilimia 3.5.
Na.Faustine Gimu Galafoni,Dodoma.
Mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Mwezi Juni,2019 umeongezeka hadi asilimia 3.7% kutoka asilimia 3. 5% kwa mwaka ulioishia Mwezi MEI,2019.
Hayo yamesema leo Julai 8,2019 jijini Dodoma na mkurugenzi wa Takwimuza Uchumi Bw.Daniel Masolwa ambapo amesema hali hiyo inamaanisha kuwa ,kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma kwa mwaka ulioishia mwezi Juni ,2019 imeongezeka ikilinganishwa na kasi ya iliyokuwepo kwa mwaka ulioishia Mwezi Mei,2019.
Bw.Masolwa amesema kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia Mwezi Juni ,2019 kumechangiwa kuongezeka kwa bei za baadhi ya bidhaa za vyakula na bidhaa zisizo za vyakula kwa kipindi kilichoishia Mwezi Juni,2019 Zikilinganishwa na bei ya bidhaa za mwaka ulioishia mwezi Juni,2018.
Baadhi ya bidhaa za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa Mwezi Juni,2019 ni pamoja na unga wa mahindi kwa asilimia 3.6%,unga wa ngano kwa asilimia 4.4%,mtama kwa asilimia 4.9%,samaki wabichi kwa asilimia 27.3%,dagaa kwa asilimia 16.5%,mafuta ya kupikia kwa asilimia 9.5%,maharagwe kwa asilimia 3.0%,mihogo kwa asilimia 16.6% na viazi mviringo kwa asilimia 18.8%.
Aidha,Bw.Masolwa amevitaja baadhi ya bidhaa zisizo za vyakula zilizochangia kuongezeka kwa mfumuko wa bei wa Mwezi Juni,2019 ni pamoja na dizeli kwa asilimia 11.4%,petrol kwa asilimia 4.9,gharama za kulala kwenye nyumba za wageni kwa asilimia 5.8% na vitabu vya shule kwa asilimia 2.4%.
Mfumuko wa bei wa bidhaa za vyakula na vinywaji baridi kwa mwaka ulioishia mwezi Juni,2019 umeongezeka hadi asilimia 2.3kutoka asilimia 2.2% kwa mwaka ulioishia mwezi Mei,2019.
Hata hivyo,Mkurugenzi huyo wa Takwimu za Uchumi Bw.Masolwa amezungumzia mfumuko wa bei kwa nchi za Afrika Mashariki kwa mwaka ulkioishia Mwezi Juni,2019 ambapo nchini Uganda mfumuko wa bei umeongezeka kwa asilimia 3.4% kwa mwaka ulioishia Mwezi Juni,2019 Kutoka asilimia 3.3% kwa mwaka ulioishia Mwezi Mei,2019 na Kenya mfumuko wa bei kwa mwaka ulioishia Mwezi Juni,2019 umeongezeka hadi asilimia 5.70% kutoka asilimia 5.49 kwa mwaka ulioishia mwezi Mei,2019.
Ikumbukwe kuwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu [NBS]ni Taasisi ya Umma iliyoanzishwa kwa sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 pamoja na mapitio yake ya mwaka 2018 na kwa mujibu wa sheria hiyo ,NBS imepewa mamlaka ya kutoa ,kusimamia na kuratibu upatikanaji wa taarifa za Takwimu hapa nchini ikiwa ni pamoja na takwimu za mfumuko wa bei kwa ajili ya matumizi ya serikali na wadau wa Takwimu.