Rais Magufuli aagiza shule zote kufunguliwa Juni 29

0
12

Rais wa Tanzania, Dkt. Magufuli ameagiza shule zote zilizokuwa zimefungwa kutokana mlipuko wa virusi vya corona zifunguliwe Juni 29, 2020.

Aidha, ameruhusu kurejea kwa shughuli nyingine zilizokuwa zimezuiwa kama watu kufunga ndoa, huku akiwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu (Covid-19).

Rais Magufuli ametoa maelekezo hayo wakati akitoa hotuba ya kufunga Bunge la 11 hafla iliyofanyika mjini Dodoma, ikiwa ni mwanzo wa maandalizi kuelekea uchaguzi mkuuu utakaofanyika Oktoba 2020.

Rais ameruhusu wananchi kuendelea na shughuli zao za kila siku kutokana na kupungua kwa maambukizi ya ugonjwa huo.

Kwa mujibu wa taarifa ya mwenendo wa ugonjwa huo hapa chini, iliyotolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa bungeni Juni 15, 2020 wakati akifunga shughuli za mkutano wa 19 wa Bunge imeeleza kuwa kuna wagonjwa 66 tu nchini, ambao wapo katika mikoa 10.

Machi 16 mwaka huu Majaliwa alitangaza kufunga shule zote na taasisi nyingine za elimu pamoja na kuzuia shughuli zinazohusisha mikusanyiko ya watu kufuatia kuripotiwa kwa muathirika wa kwanza wa corona nchini Machi 15, 2020, ambaye aliripotiwa mkoani Arusha.

Mei 21 mwaka huu Rais Magufuli alitangaza uamuzi wa kufungua vyuo vikuu, kurejea masomoni kwa wanafunzi wa kidato cha sita, na kurejea kwa shughuli za michezo kuanzia Juni 1, ambapo pia alisema ataangalia mwenendo wa hali, ili kuamua wakati gani wa kufungua shule za sekondari, msingi na awali.

Send this to a friend