Mtandao wa WhatsApp wazindua huduma ya kutuma na kupokea fedha
Baada ya miezi kadhaa ya mazungumzo na majaribio, mtandao wa WhatsApp umezindua huduma ya malipo kupitia programu tumishi hiyo.
Mtandao huo wa kutumiana jumbe unaomilikiwa na Facebook umetangaza kuwa watumiaji wake wa Brazil ndio walioanza kutumia huduma hiyo ya kutuma na kupokea fedha kwa kutumia Facebook Pay, huduma ya malipo ambayo Facebook iliizindua mwaka 2019.
WhatsApp imesema kuwa huduma hiyo ni bure kwa watumiaji wa kawaida, lakini wanaotumia kwa masuala ya biashara watalipa ada 3.99% kupokea malipo, na itahitaji tarakimu sita (PIN) au alama za kidole kukamilisha muamala.
Kwa nchini Brazil ambapo majaribio yameanza, watumiaji wanatakiwa kuunganisha WhatsApp zao na Visa, Mastercard credit au debit card, pamoja na watoa huduma wa ndani (nchini humo) ambao ni Banco do Brasil, Nubank na Sicredi ili kukamilisha miamala.
Taarifa hiyo imekuja kwa kushtukiza kwani kwa muda sasa WhatsApp imekuwa ikifanya majaribio ya huduma ya malipo nchini India kwa kutumia UPI badala ya Facebook Pay.
Nchini Tanzania na maeneo mengine duniani WhatsApp imekuwa ikitumika kibiashara ambapo baadhi ya watu hutumia huduma ya WhatsApp Business, huku wengine wakitumia WhatsApp ya kawaida lakini wakituma picha, video na maelekezo mengine kuhusu bidhaa na huduma wanazotoa.
Kwa kuanzishwa kwa mfumo wa malipo, WhatsApp yenye watumiaji zaidi ya bilioni 2, itawezesha kutumika zaidi kwenye biashara kwa kuwapa watu si tu nafasi ya kutumiana jumbe kuhusu biashara au taarifa za miamala, lakini kufanya miamala.
Mtandao huo umewatoa hofu watumiaji wake kwamba watakapofanya malipo baaada ya kutumia huduma au kununua bidhaa, mawasiliano yao (chat) zitaendelea kuwa salama na siri