TFF yaweka wazi sababu ya kutohudhuria kikao cha Waziri Dk Mwakyembe

0
27

Tumesikia taarifa kupitia vyombo vya habari ya kuwa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF), limeshindwa kuhudhuria kikao kilichoitishwa na Waziri wa Habari,Sanaa,Utamaduni na Michezo,Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe kilichotakiwa kufanyika Julai 9,Uwanja wa Taifa Dar es Salaam,mwaka huu.

TFF inakiri kupokea  ,mualiko wa kikao cha Mheshimiwa Waziri  kilichotakiwa kufanyika Julai 8,ambapo baadaye kilibadilishwa na kuwa Julai 9,vikao vyote hivyo viwili tulithibitisha ushiriki wetu  kabla ya kupata taarifa zingine tena kutoka kwa wasaidizi wake ya  kuwa kikao hicho kimesogezwa mbele tena hadi  Julai 10 mwaka huu

Baada ya kupata taarifa hiyo tulijibu kupitia wasaidizi wa Mh Waziri, kuwa viongozi wa TFF wamebanwa na ratiba nyingine muhimu na nzito sana ambazo tayari zipo kwenye makubaliano na kuomba kupangiwa muda mwingine wa kikao kwa Mheshimiwa Waziri.

Tuliwaeleza wasaidizi wake  kuwa Katibu Mkuu wa TFF Wilfred Kidao atakuwa na ratiba ya ukaguzi  kutoka FIFA kwa ajili ya ukaguzi wa fedha za FIFA kwa mwaka 2018,ratiba ambayo tayari ilikwishapangwa kwa pamoja tangu  Januari  Mosi mwaka huu ,

Pia,tuliwajulisha ya kuwa Rais wa TFF,Wallace Karia yupo nchini Rwanda  pamoja na Kaimu Makamu wa Rais Athuman Nyamlani atakuwa na kikao cha makubaliano na uongozi wa Fountain Gate Academy kuhusiana na timu zetu za taifa za Vijana.

Kikao hicho cha makubaliano na Fountain Gate Academy,tulikihairisha kukifanya kutokana na tarehe hizo kugongana na tarehe ambazo Mheshimiwa Waziri aliomba awali kufanya vikao na TFF,hivyo kutokana na mmiliki wa Fountain Gate Academy kuwa na safari za kikazi,tulishindwa kubadilisha tarehe ya kukutana nao.

Tuliwapa taarifa viongozi wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT) ,kuwa tutashindwa kuhudhuria mualiko huo,kutokana na sababu hizo tulizoziainisha hapo juu.TFF kwakuwa ilishatoa taarifa kwa chombo kilichotupa taarifa za kikao, tuliamini Mheshimiwa Waziri alipata taarifa sahihi za kutokuhudhuria kwetu.

Pia,tungependa kuufahamisha umma kuwa tumekuwa na vikao  vya mara kwa mara na Waziri mwenye dhamana  ya Michezo kujadiliana kuhusiana na masuala yahusuyo  mpira wa miguu  na hata zilipokuwa zikitokea changamoto  alitutumia taarifa  nyakati za  jioni na kutakiwa kufika Dodoma asubuhi inayofuata,lakini tumekuwa tukitii maagizo hayo ya Waziri kuwahi vikao hivyo.

Baada ya kikao cha jana kushindwa kufanyika kutokana na kutohudhuria,tulipata taarifa nyingine ya kututaka kuhudhuria kikao kingine,jambo ambalo TFF  tunaamini ndio njia sahihi ya kufanya kazi kati ya TFF na Wizara yenye dhamana ya Michezo.

Taasisi inapenda kuujulisha umma kuwa makubaliano ya kuvunja mkataba na kocha Emmanuel Amunike yalikuwa ya pamoja baina ya pande mbili,hivyo TFF itatoa taarifa kamili kuhusiana na makubaliano hayo ya kusitisha  mkataba na kocha Amunike, ambapo maamuzi hayo yalitokana baada ya mazungumzo ya msingi  baina ya TFF na kocha.

Tunaamini tutaendelea kufanya kazi na Wizara hiyo yenye dhamana ya michezo kama tulivyokuwa tukifanya nao mara zote na hasa ikizingatiwa kuwa Serikali ni mdau mkubwa wa mpira wa miguu nchini.

TFF imekuwa ikishirikiana na Mamlaka mbalimbali za Serikali kwa kuamini Serikali ni mdau Mkuu wa mchezo wa mpira wa miguu na itaendelea kushirikiana na Mamlaka  zenye nia njema na Maendeleo ya Mpira wa Miguu.

Send this to a friend