Uchaguzi Mkuu Tanzania 2020: Wasifu wa Balozi Ali Karume

0
26

Na Farid Hashim, Zanzibar

Kinyang’anyiro cha mbio za Urais Zanzibar ndani ya CCM kimepamba moto baada ya makada zaidi ya 10 kujitokeza na kuchukua fomu kuomba ridhaa. Mmoja wa waliochukua fomu ni Balozi Ali Abeid Amani Karume. Balozi Karume alikabidhiwa fomu hizo Juni 15 katika ofisi za CCM Kisiwandui Unguja. 

Historia ya Balozi Karume inaonesha kwamba alizaliwa Mei 24 mwaka 1950 Kisima Majongoo, Unguja Zanzibar. Kitaaluma Balozi Karume ni Mchumi na Mwanadiplomasia. 

Kielimu, Balozi Karume alihitimu elimu yake ya Msingi mwaka 1963 katika Shule ya His Highness The Aga Khan, Zanzibar. Elimu yake ya Sekondari ya Kidato cha Kwanza hadi cha Nne aliipata katika Sekondari ya Mtakuja iliyopo Zanzibar na kisha kuhitimu Kidato cha Sita mwaka 1969 Lumumba College, Zanzibar. Mwaka 1982 alihitimu Shahada ya Uchumi na Siasa toka Chuo Kikuu cha Columbia kilichopoa New York nchini Marekani. Balozi Karume pia ana Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uchumi wa Biashara. 

Kwa upande ajira, wasifu wake unaonesha kwamba alianza kazi mwaka 1969 kama Naibu Mkurugenzi ZSTC Zanzibar hadi mwaka 1971 alipopanda cheo na kuwa Mkurugenzi katika shirika hilo. Mwaka huo huo wa 1972 akateuliwa kuwa Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar. Alidumu katika wadhifa huo kwa miaka 6, hadi mwaka 1978. Baadaye Balozi Karume akaingia katika diplomasia na kati ya mwaka 1985 hadi 1989 akahudumu kama Naibu Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji. Kuanzia 1989 hadi 1993, akawa Naibu Balozi wa Tanzania nchini Marekani kabla ya kurudi Tanzania  na kuwa Balozi na Mkurugenzi Wizara ya Mambo ya Nje kwenye Ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje jijini Dar es Salaam. Alikaa katika nafasi hiyo kuanzia mwaka 1993 hadi 1995.

Ushiriki wake katika kazi za Kidiplomasia ukamuondoa tena Tanzania na kumpeleka Ulaya ambako kuanzia mwaka 1995  hadi 2002 aliiwakilisha Tanzania kama Balozi katika nchi za Ubelgiji, Uholanzi, Luxembourg na Jumuiya ya Ulaya. Mwaka 2002 hadi 2006 akateuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Ujerumani, Uswisi, Austria, Poland, Czech Republic, Slovakia, Hungary – Romania, Bulgaria, na Vatican.2006 hadi 2011 akawa Balozi wa Tanzania Italia, Uturuki, Ugiriki, Slovenia, Malta na Cyprus. Kati ya mwaka 2007 hadi 2008 alikuwa Mkuu wa Mabalozi wa Tanzania walioko nchi mbalimbali duniani. 

Ndani ya CCM, Balozi Karume amekuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mkoa wa Kusini Unguja kuanzia mwaka 2012 hadi 2017. Amekuwa pia Mjumbe wa Kamati ya Siasa CCM, Mkoa wa Kusini Unguja na Mjumbe wa Kamati ya Siasa CCM, Wilaya ya Kati, Unguja.

Balozi Karume ni mmoja ya makada wa CCM zaidi ya 10 ambao mpaka sasa tayari wamechukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea Urais wa Zanzibar. Makada wengine ni Profesa Makame Mnyaa Mbarawa, Mbwana Juma, Shamsi Nahodha, Omari Musa, Meja Jenerali mstaafu Suleiman Nassor, Mohamed Hija, Dkt Hussein Mwinyi, Mohamed Jumanne na Mbwana Yahya. Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM wanatarajiwa kufanya uteuzi wa kada mmoja kwenye nafasi hiyo Julai 12 2020. 

Send this to a friend