Msimamo wa Bernard Membe kuhusu kugombea Urais wa Tanzania
Aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe amesema kuwa atagombea nafasi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2020 endapo tu Chama cha Mapinduzi kitabatilisha adhabu aliyopewa.
Akizungumza na wakazi wa Lindi mapema mwishoni mwa wiki hii, Membe amesema endapo adhabu hiyo haitotolewa hatoweza kugombea kwa sababu anaweza asipewe fomu au asipate ushirikiano mikoani na wilayani ambapo atahitajika kwenda kutafuta wadhamini.
“Kwa kuwa chombo kinachotoa adhabu ni Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), na kwa kuwa Kamati ya Maadili tayari imeandaa taarifa yake na wameipitisha kwenye Kamati Kuu na kwa bahati mbaya kamati kuu ikatamka kwamba Membe tumemfukuza. Mpaka hapo Halmashauri Kuu [ya CCM] iatakaposema mheshimiwa Membe hana hatia, wakitamka hivyo leo [jana] au wakitamka hivyo kesho [leo] tutajaza kugombea Urais jumatatu asubuhi,” amesema Membe.
Amesema endapo Kamati Kuu ya CCM itakataa kubatilisha adhabu hiyo ambayo amesema kwa usahihi ilitakiwa kutolewa na Halmashauri Kuu ya CCM (itakutana Julai 2020), hatogombea.
“Ikikataa, huwezi mimi kunituma niende Dodoma. Nikienda kule, nikikataliwa kuchukua fomu? Je! Nikipewa ile fomu nakaenda kwenye mkoa au wilaya nisimkute anayehusika…, haitawezekana,” ametahadharisha.
Aidha, amewataka vijana na wananchi kutokusababisha vurugu badala yake wahakikishe kuna utulivu wa kutosha, kwani lengo ni kuwa na uchaguzi wenye amani.
Membe alifukuzwa uanachama wa CCM Februari 28 mwaka huu na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM kutokana na kutobadili muenendo wake ndani ya chama tangu mwaka 2014 licha ya kupewa adhabu zilizolenga kumrekebisha.
Tayari wanachama wa vyama mbalimbali wamejitokeza kuchukua fomu za kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera za vyama vyao katika kugombea nafasi ya Urais wa Tanzania pamoja na Zanzibar.