Tanzania yaamriwa kuwalipa fidia wafungwa 10 raia wa Kenya
Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu imeiamuru serikali ya Tanzania kuzilipa fidia familia za raia 10 wa Kenya waliohukumiwa kifungo nchini.
Katika hukumu iliyotolewa na mahakama hiyo Julai 4 mwaka huu, ilielezwa kwa wafungwa hao wanastahili fidia kutokana na kesi hiyo kuendeshwa kwa muda mrefu tofauti na ilivyotakiwa.
Hukumu hiyo ilitolewa katika kesi iliyofunguliwa na raia wa Kenya dhidi ya serikali ya Tanzania kufuatia kukamatwa kwao jijini Maputo nchini Msumbiji, na mchakato mzima wa kesi uliofuata.
Mbali na kulalamika kuwa kesi ilichukua muda mrefu tofauti na ilivyotakiwa, walieleza kuwa mamlaka nchini Tanzania zilikiuka haki zao.
Raia hao waliohukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa wizi wa kutumia nguvu ni Wilfred Onyango Nganyi maarufu Dadii, Peter Gikuru Mburu maarufu Kamau, Jimmy Maina Njoroge maarufu Ordinary na Patrick Mutheee Muriithi maarufu Musevu.
Wengine ni Simon Githinji Kariuki, Boniface Mwangi Mburu maarufu Bonche, David Ngigu Mburu maarufu Mike, Gabriel Kungu Kariuki, John Odongo Odhiambo na Simon Ndungu Kiambuthi maarufu Kenen.
Washtakiwa watano waliachiwa huru kutokana na kukosea kwa ushahidi dhidi yao wa kuwatia hatiani.
Majaji 11 wa mahakama hiyo iliyopo jijini Arusha wakitoa hukumu hiyo walisema kuwa walalamikaji hawakueleza kama madhara waliyoyapata kutokana na ukiukwaji wa haki zao yalikuwa tofauti kutoka kwa mtu mmoja na mwingine.
Majaji hao walisema kuwa kesi hiyo ilichukua miaka 2 miezi 6 na siku 14 kinyume na maagizo yaliyotolewa na mahakama ya juu ambayo iliagiza kesi hiyo kuendeshwa kwa haraka.
Pia walitilia maanani kuwa wafungwa hao walipata madhara wakati waliokuwa wakishikiliwa kabla ya kesi yao kuanza kusikilizwa.
Katika fidia hiyo, mahakama iliamuru kuwa itatolewa kwa ndugu wa karibu wa mfungwa ambao ni baba, mama, mke/mume au watoto.
Hata hivyo majaji walitupilia mbali kiasi cha fidia ambao wafungwa hao walitaka ndugu wa karibu walipwe ambacho ni, mke (mume) alipwe TZS 2.3 milioni, kila mtoto TZS 1.8 milioni na mama au baba (mtegemezi) TZS 1.2 milioni.
Kwa madhara ya kimwili na kiakili kwa wale waliochiwa huru mahakama iliamuru walipwe TZS 6.9 milioni, huku wale 10 waliofungwa walipwe TZS 9.2 milioni.
Pia majaji walitoa fidia ya TZS 300,000 kwa kila mfungwa kama gharama za masuala ya kisheria katika muda wote wa kesi, lakini mahakama ilikataa kuwafutia hukumu yao.
Mahakama pia ilikataa kuamuru walipwe fidia kwa kupoteza kipato (loss of income) muda wote waliokuwa wakishikiliwa, kwa sababu hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha hilo.
Hata hivyo serikali imesema fidia hizo hazina mashiko.