CCM yamjibu Membe ombi la kutaka kugombea Urais wa Tanzania

0
22

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa hatma ya uanachama wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe ilishamalizika alipofukuzwa uanachama mapema Februari mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa (wa CCM), Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga wakati akizungumza na Gazeti la The Citizen siku chache baada ya mwanachama huyo kuonesha nia ya kutaka kugombea Urais wa Tanzania.

Akizungumza akiwa mkoani Lindi, Membe alisema kuwa pendekezo la Kamati Kuu ya CCM (CC) kwamba afukuzwe uanachama bado halijapitishwa na Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) kama katiba ya chama hicho inavyotaka.

“Ukweli ni kwamba ameshafukuzwa uanachama, asubiri aone kama atasamehewa, au aombe uanachama upya. Ajue kuwa hatusumbuliwi wala hatuogopeshwi na maneno yake,” amesema Kanali Lubinga.

Katika mkutano wake, Membe alisema kuwa endapo NEC itabatilisha adhabu aliyopewa na Kamati Kuu na kusema kuwa hana hatia, atachukua fomu ya kuomba ridhaa ya CCM kugombea Urais wa Tanzania katika uchaguzi ujao.

Membe ni mtu kwa kwanza kusema hadharani kuwa anataka kuchuana na Rais Magufuli ndani ya chama hicho katika kuwania kuteuliwa kupeperusha bendera ya chama.

Rais Magufuli ambaye ndiye Mwenyekiti wa CCM Taifa juma lililopita alichukua fomu ya kuomba ridhaa ya chama hicho kugombea muhula wa pili, na hadi sasa ndiye mwanachama pekee aliyechukua fomu.

Send this to a friend