Mchimbaji mdogo aibuka na mawe ya Tanzanite yenye thamani ya bilioni 7.8
Kuna msemo wa Kiswahili ambao husema “Mtafutaji Hachoki,” na wengine huongezea kuwa akichoka ujue kapata.
Huo ndio msemo unaoweza kutumika kuelezea hali ya mchimbaji mdogo wa madini ya Tanzanite, Saniniu Laizer ambaye amekuwa bilionea baada ya kupata madini yenye thamani kubwa.
Taarifa ya Wizara ya Madini imeeleza kuwa Laizer amepata mawe mawili makubwa yenye thamani shilingi 7.8 bilioni.
Kati ya mawe hayo mawili aliyopata mchumbaji huyo, moja lina uzito wa 9.2kg ambalo lina thamani ya TZS 4.5 bilioni na la pili lina 5.8kg lenye thamani TZS 3.3 bilioni.
Kufuatia tukio hilo, Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila amesema kuwa leo Wizara inamtabua Mchimbaji mdogo wa madini ya Tanzanite Bw. Saninniu Laizer kuwa bilionea.
“Na utofauti wake ni kwamba mawe ya uzito huo hayajawahi kupatikana kwenye machimbo ya tanzanite tangu machimbo yaanze na yamepatikana ndani ya ukuta wa Mirereni kwahiyo hii ni rekodi mpya ya kupata mawe yenye uzito huo,” amesema Prof. Msanjila.