TCRA yavitoza faini milioni 30 vituo 6 kwa kurusha maudhui yasiyofaa

0
29

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imevitoza faini ya TZS 30 milioni vituo sita vya utangazaji vikiwemo vya mitandaoni kutokana na kukiuka kanuni na maadili ya utangazaji.

Akitoa taarifa kwa vyombo vya habari Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Joseph Mapunda amesema vyombo hivyo vilikiuka kanuni za utangazaji kwa nyakati tofauti.

Vituo vilivyotozwa faini pamoja na kupewa adhabu nyingini ni Clouds FM ambayo imetozwa faini ya TZS 5 milioni na kupewa onyo kali kwa kosa la kuzungumzia supu ya pweza inavyoimarisha tendo la ndoa katika muda ambao wasikilizaji wanaweza kuwa watoto.

Vituo vingine ni East Africa Radio ambayo imetozwa faini TZS 7 milioni na onyo kali kwa kosa la kukashifu utendaji wa serikali kutokana na uteuzi wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Kituo cha tatu ni Global TV ambayo imetozwa faini TZS 7 milioni na onyo kali kwa kurusha maudhui yasiyo na lugha ya staha huku Duma TV imetozwa faini TZS 7 milioni na kufungiwa kwa mwezi mmoja kutokana na kurusha maudhui ya unyanyasaji wa kijinsia.

Kituo cha tano ni Sibuka TV imetozwa faini TZS 3 milioni na onyo kali kwa kosa la kurusha maudhui ya kushabikia mauaji. Kituo cha sita ni Star TV ambayo imetozwa faini TZS 5 milioni na kutakiwa kuomba radhi kwa siku tatu kutokana na kukashifu viongozi wa Wilaya ya Kisarawe.

Send this to a friend