Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimechagua maji matano miongoni mwa majina 32 ya watia nia waliokuwa wanaomba ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho kugombea Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.
Akizungumza baada ya kikao cha Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya CCM, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Abdallah Juma Mabodi amesema mchakato wa kuwachagua watu hao umefuata taratibu zote za chama hicho.
Babodi amesema miongoni mwa vigezo walivyotumia kuwachagua watia nia watano ni pamoja na elimu zao, maeneo walipozaliwa na uwezo wao.
Amesema kuwa baada ya hatua hiyo, majina hayo matano yatapelekwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM, na kamati hiyo itapeleka kwenye Halmashauri Kuu ya CCM majina matatu ambayo itateua mgombea.
Tanzania inatarajia kufanya uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge, Madiwani na Wawakilishi Oktoba mwaka huu.