Rais aagiza uchunguzi wa matumizi ya TZS 15.3bn za TAZARA
Rais Dk Magufuli ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kuchunguza matumizi ya shilingi Bilioni 15 na Milioni 300 zilizotolewa na Serikali kwa ajili ya kugharamia matumizi ya Mamlaka ya Usafiri wa Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Ametoa agizo hilo leo tarehe 26 Julai, 2019 wakati akizungumza na wafanyakazi na abiria katika kituo kikuu cha TAZARA Jijini Dar es Salaam muda mfupi baada ya kuwasili kwa treni ya TAZARA kutoka Fuga Mkoani Pwani akitokea Rufiji ambako ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji.
Fedha hizo zilitolewa na Serikali katika mwaka wa fedha wa 2017/18 na 2018/19 kwa ajili ya matengenezo ya injini 7 ambazo zingewezesha kumudu kusafirisha tani 400,000 za mizigo, kugharamia ukarabati mkubwa na ununuzi wa mitambo mipya ya mgodi wa kokoto za ujenzi wa reli na kuboresha miundombinu ya reli katika stesheni ya Fuga.
Pamoja na kutoa maagizo hayo, Mhe. Rais Magufuli amewahakikishia wafanyakazi wa TAZARA kuwa Serikali haiwezi kuiacha TAZARA ife na kwamba atazungumza na Rais wa Zambia Mhe. Edgar Lungu ili kwa pamoja wachukue hatua madhubuti za kuimarisha miundombinu na kununua injini na mabehewa.
“Nimesafiri na treni ya TAZARA nimejionea mwenyewe, nataka niwahakikishie sasa nitaelekeza nguvu zangu TAZARA” amesema Rais Magufuli.
Kwa sasa TAZARA ambayo reli yake ina uwezo wa kusafirisha tani Milioni 5 kwa mwaka inahitaji injini 15 za treni ya mizigo, injini 4 za treni ya abiria na mabehewa 700 ili iweze kusafirisha angalau tani laki 6 za mizigo kwa mwaka zitakazozalisha faida, ikilinganishwa na hali ilivyo hivi sasa ambapo inasafirisha tani 250,000 tu kwa mwaka.
Akiwa njiani kufika kituo kikuu cha TAZARA, Mhe. Rais Magufuli amesimama katika eneo la Mwakanga (Kigogo Fresh) Wilayani Ilala na baada ya wananchi kudai hawajengewa choo wala kupelekewa maji katika soko lao licha ya kuomba mara kadhaa, ameagiza kuanzia sasa wasilipe ushuru wa soko wa shilingi 500 kila siku mpaka hapo Manispaa itakapowajengea choo na kuwapelekea maji.