Mzee Butiku: CCM iachane na rushwa kwenye uchaguzi

0
32

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere amekitaka Chama cha Mapinduzi (CCM) ambacho na yeye ni mwanachama kioneshe mfano kwa kuongoza kupinga vitendo vya rushwa katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Mzee Joseph Butiku ametoa kauli hiyo katika mahojiano na TBC ambapo ameeleza kuwa anafahamu kwamba kuna rushwa ndani ya chama hicho ndio sababu anakiasa kibadilike.

“Niombe CCM chama changu kiongoze kuachana na rushwa, najua ipo, na kimsaidie Rais Magufuli kufuta rushwa katika uchaguzi huu,” amesema Butiku.

Katika hatua nyingine amewaasa wale wote watakaoteuliwa kugombea ngazi mbalimbali za uongozi wafahamu kuwa hawatafuti kazi bali wanaomba kuwa tumikia wananchi.

Ameasa kuwa endapo yeyote kati ya wateuliwa atakuwa anagombea ili ajipatie mali, ufahari au jambo jingine kwa maslahi yake mwenyewe, asigombee kwani hafai kuwa kiongozi.

“Wanaogombea wafahamu kuwa wanakwenda kuomba uongozi, sio kutafuta kazi. Huwezi ukasema unawaongoza watu hawana viatu halafu wewe una jozi 200. Kama unagombea kupata gari au mke wa pili, usiende,” ametoa rai hiyo.

Amesema uongozi ni kuwasaidia watu kupata gari hata kama kiongozi hana gari, na kwamba dhana pana ya uongozi inamtaka kiongozi awe mtu wa mwisho kula baada ya wale anaowaongoza.

Send this to a friend