Serikali yapiga marufuku walimu kuingia na viboko darasani
SERIKALI imepiga marufuku walimu wanaofundisha madarasa ya kuanzia elimu ya awali hadi darasa la tatu kuingia na viboko darasani.
Kauli hiyo imetolewa juzi mjini Mwanza na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) anayeshughulikia elimu, Tixon Nzunda wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha kuandaa vipindi vya redio kupitia Mpango wa Kuinua Ubora wa Elimu Tanzania (MKUE-Tanzania).
Nzunda alisema kuwa vitendo hivyo vinasababisha wanafunzi wa madarasa hayo kuogopa na kutokuwa wasikivu wakati wanapofundishwa.
Kanuni ya 3(1) ya Sheria ya Elimu, Sura ya 353, marejeo ya mwaka 2002, inasema adhabu ya viboko itatolewa iwapo patatokea utovu mkubwa wa nidhabu au kosa kubwa litakalofanywa ndani au nje ya shule ambalo litaishushia shule heshima.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, kanuni ndogo ya (2) inasema adhabu ya viboko itolewe kwa kuzingatia umri, jinsia na afya ya mwanafunzi na isizidi viboko vinne kwa tukio lolote.
Sheria inamtaka mwalimu mkuu wa shule husika kutoa adhabu ya viboko au kukasimisha mamlaka yake kwa umakini mkubwa kwa mwalimu yeyote kutoa adhabu hiyo.
Katika hatua nyingine, Nzunda ametoa wito kwa wadau wa elimu kushirikiana na Serikali katika kujenga mazingira mazuri ya utoaji elimu nchini ikiwemo ujenzi wa madarasa, vyoo na nyumba za walimu.
Alisema hali ilivyo sasa, ili kukamilisha miundombinu na kuweka mazingira mazuri ya utaoji elimu na ujenzi wa nyumba za kuishi walimu, zinahitajika Sh trilioni 14 kutekeleza hilo katika shule za sekondari na msingi nchini kote.
Nzunda alisema Serikali peke yake haiwezi kukamilisha hilo bila kushirikiana na wadau wengine kujenga madarasa ya kutosha ili kupunguza msongamano wa wanafunzi, kuondoa uhaba wa nyumba za walimu na vyoo.