Mzee Mwinyi ataka Rais Magufuli aongezewe muda kuongoza
Rais Mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa licha ya kuwa nchi inaongozwa kwa katiba, lakini inaweza kubadilishwa endapo itaridhiwa, ambapo amependekeza ifanyike hivyo ili kumruhusu Rais Dkt. Magufuli kuendelea kushika wadhifa huo.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Mzee Mwinyi amependekeza Rais Magufuli apewe muhula mmoja wa nyongeza wa asante kwa mambo makubwa aliyofanya, lakini ikiwezekana baada ya hapo aruhusiwe kuongoza hadi dunia iishe.
“Nchi yetu inaendeshwa kwa katiba na katiba lazima tuienzi, tusiingilie, lakini twaweza tukitaka. Twaweza kuiahirisha kwa muda mfupi ili kumpa Rais wetu huyu kipindi kimoja cha asante. Tukisha[maliza], tuendelee mpaka dunia iishe kwa sababu kuna mengi aliyonayo na nchi itayakosa vinginevyo,” amesema Mzee Mwinyi.
Akijibu hoja hiyo, Rais Dkt Magufuli amemuuliza Rais Mwinyi kwanini yeye hakuongeza muda alipomaliza kipindi chake, au Rais Jakaya Kikwete na Rais Benjamin Mkapa, mbona wao hawakuongeza muda.
Mkutano huo unaoendelea katika ukumbi wa CCM jijni Dodoma pamoja na mambo mengine unakusudia kupiga kura ya kumpitisha mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.