Wakazi wa Kilimanjaro kumuomba radhi na kumpa tuzo Rais Magufuli

0
24

Na Dixo Busagaga ,Moshi

Wazee katika mkoa wa Kilimanjaro wakiwemo viongozi wa mila, machifu na malaigwanani wameanza mchakato wa kumpongeza na kumpa tuzo maalumu Rais Dkt. Magufuli kwa kazi aliyofanya katika kipindi cha miaka mitano.

Katika tukio hilo wananchi wenye asili ya Kanda ya Kaskazini wanakusudia pia kumuomba radhi Rais Magufuli kutokana na maamuzi waliyofanya wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 kwa kumpa kura chache.

Mwenyekiti wa kamati inayoratibu mchakato huo, Yunusi Mmari amesema maandalizi ya tukio hilo tayari yameaza huku yakishirikisha wazee kutoka wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro.

“Kusudio la tukio hili ni kuwakutanisha wazee kutoka wilaya zote za Mkoa wa Kilimanjaro na mikoa ya jirani wakiwemo wazee wa mila kama Machifu na Malaigwanani ambao watakuwa na ujumbe maalumu wanaotarajia kuufikisha kwa Rais Dkt Magufuli,” amesema Mmari .

Kwa upande wake Joseph Msele ambaye ni katibu amesema watu wengi wamejiandaa kushiriki huku kamati kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali vikiangalia eneo kubwa zaidi la kufanyika kwa tukio hilo.

“Ni kweli imekua kiu ya wengi kutamani kumpatia Rais Magufuli tuzo na sisi kazi yetu kama kamati ni kuratibu tu hayo mawazo ya wengi ili kuyafikisha kwenye kilele hicho.”

Tukio la pogezi na utoaji tuzo kwa Rais Magufuli linataraji kupambwa na vikundi vya ngoma za asili ambavyo vimekuwa sehemu ya maandalizi ya tukio hilo.

Send this to a friend