Viongozi wa CHADEMA wakamatwa kwa kuingia Morogoro Kusini bila kibali cha Polisi

0
15

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimeripoti kuwa Jeshi la Polisi mkoani Morogoro limewakamata viongozi wake kwa madai kuwa wameingia pasi na kuwa na kibali cha Polisi.

Kupitia ukurasa wa Twitter, chama hicho kimeeleza kuwa Polisi walisimamisha gari la chama likiwa barabarani na kuwakamata viongozi wanaosimamia CHADEMA ni Msingi na uchaguzi wa chama mkoani humo, wakidaiwa kutenda kosa la kuingia Jimbo la Morogoro Kusini bila ruhusa ya Polisi.

CHADEMA kimewataja waliokamatwa kuwa ni Naftal Ngogo, Jackson Malisa na Dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo ambaye ametajwa kwa jina moja la Leonard.

Chama hicho kimesema licha ya viongozi hao kukamatwa eneo la Matombo, hawakuelezwa sababu ya kukamatwa kwao hadi walipofika kwa Kamanda wa Polisi wa Wilaya (OCD).

Hata hivyo baada ya kufika katika ofisi ya OCD, polisi waliamriwa wawapeleke katika Kituo cha Polisi Morogoro Mjini.

Chama hicho kimesema kuwa shughuli za uchaguzi wa chama na CHADEMA ni Msingi zinaendelea nchi nzima na Jeshi la Polisi linazo taarifa za shughuli hizo.

Juhudi za Naftal Ngogo kumkumbusha OCD kuwa ofisi yake inazo taarifa na kwamba hawakuhitaji kibali, pia kuwa wamekamatwa wakiwa njiani wakipeleka fomu za uchaguzi hazijafanikiwa, chama hicho kimeeleza.

Kwa sasa chama hicho kimesema kuwa kimetuma mwanasheria kwenda kusimamia suala hilo.

Send this to a friend