Balozi Dk Slaa awakosoa wanaotumia mitandao kuichafua serikali
Balozi wa Tanzania nchini Sweden Dkt. Wilbrod Slaa amekemea tabia ya Watanzania kuweka mambo ya ndani ya nchi kwenye mitandao ya kijamii, na kubeza utendaji wa serikali, akisema mambo hayo yanawapa shida mabalozi kuitetea nchi huko walipo, kwa sababu yanawakatisha tamaa wahisani wanaotaka kuisaidia au kuja Tanzania
Dkt. Slaa ametoa kauli hiyo wakati akifanya mahojiano na kituo cha runinga cha Star TV wakati wa ziara ya mabalozi wa Tanzania kutoka nchi mbalimbali duniani walipotembelea mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa SGR eneo la Soga Mkoani Pwani.
Ametoa mfano kutokana na kauli aliyoitoa kongozi fulani ambaye hakumtaja, ambapo amesema ilisababisha kwa siku moja watalii 100 kutoka Sweden kuahirisha safari ya kuja Tanzania kutalii.
Amesema kama kuna tatizo la ndani ya nchi, lijadiliwe katika majukwaa ya ndani ya nchi na siyo kupeleka kwenye mitandao ya kijamii au vyombo vya habari vya kimataifa, kwani vinaichafua nchi.
Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali wapo katika ziara ya kutembelea na kuijonea utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya awamu ya tano kwa fedha za ndani.