Chama cha siasa kitakachotumia zaidi ya TZS 17 bilioni, kutoshiriki uchaguzi ujao

0
28

Sheria ya udhibiti wa matumizi ya fedha katika uchaguzi imeweka ukomo wa chama cha siasa kutotumia zaidi ya TZS 17 bilioni katika shughuli zake zote za uchaguzi Tanzania Bara na visiwani.

Hayo yameelezwa na Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza wakati akizungumza na TBC, ambapo amesema kuwa chama kitakachokiuka sheria hiyo kitazuiwa kushiriki kwenye uchaguzi unaofuata na endapo kimeshinda, ushindi wake unaweza kutenguliwa.

“Uchaguzi wote [chama] kinatakiwa kisitumie zaidi ya bilioni 17, kikivuka bila kuwa na sababu za msingi, msajili atakikatalia chama kushiriki uchaguzi unaofuata. Pia msajili anaweza kuiomba Tume ya [Taifa ya] Uchaguzi kukipa adhabu chama wagombea wake hata kama wameshinda waondoke,” amesema Sisty.

Akizungumzia suala la vyama vya siasa kupokea fedha kutoka nje ya nchi kwa ajili ya shughuli za uchaguzi amesema kwa sasa muda huo umekwisha.

“Chama cha siasa kinapaswa kupokea fedha kwa ajili ya uchaguzi miezi mitatu, siku 90, kabla ya uchaguzi. Ina maana kwa sasa hivi chama cha siasa hakiwezi kupokea fedha kutoka nje kwa ajili ya uchaguzi,” ameeleza Sisty.

Aidha, amevitaka vyama vya siasa kuzingatia sheria za uchaguzi, kanuni zake pamoja na maadili ili kujiepusha na adhabu mbalimbali zinazoweza kutolewa ikiwa ni pamoja na kufutiwa matokeo ya wagombea wake.

Send this to a friend